Siwezi Acha kuzungumza kama watu wanatekwa....Gwajima

Mbunge wa Kawe, mkoa wa Dar es Salaam Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Askofu wa Kanisa la Glory Of Christ Tanzania, Josephat Gwajima amesema hawezi kuacha kuzungumza kama watu wanatekwa.
Gwajima ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, kufuatia miezi kadhaa ya mvutano na chama chake cha Siasa tangu akemee matukio hayo mwezi Mei mwaka huu.
“Kuhusu utekaji siogopi mtu, hata kama makanisa yatafungwa kwa miaka 100, siwezi kuacha kuzungumza kama watu wanaendelea kutekwa. Hakuna kutekana, hakuna kuumizana. Sijasema CCM inateka, lakini ndiyo chama kilicho madarakani.”
Ameeleza njia pekee ya kukomesha vitendo hivyo ni kutoa ulinzi kwa wakuu wa vyombo vya usalama ili wasipate matatizo kutoka kwa wakuu wao wa kisiasa pale wanapolinda nchi. Pia ametaka vyombo vya dola viwekwe mbali na siasa.
Gwajima ameweka wazi kwamba ataihama CCM, na kuongeza kwamba bado ni mwanachama wa chama hicho na ataendelea kuwepo: “Sihami, CCM nipo sana, tunabanana humu humu ndani.”
Kwa upande mwingine amekita chama chake kufanya marekebisho madogo yatakayo wezesha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Ikumbukwe kuwa mwezi April mwaka huu Chadema ilitangaza kususia kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, na kushikilia kampeni yake ya kutaka mageuzi katika mifumo ya uchaguzi kabla ya kwenda kwenye uchaguzi huo.
Kiongozi huyo wa kisiasa na kidini ambaye wakati fulani aliwahi kuingia kwenye mivutano kwa sababu ya kutumia lugha ya kuudhi na kejeli dhidi ya viongozi wengine wa kisiasa na kidini amesema iwapo CCM inajiamini kushinda uchaguzi wa Oktoba iweke marekebisho ya mifumo ya uchaguzi na kuiruhusu Chadema kushiriki uchaguzi kisha iishinde kupitia sanduku la kura
Mei 25 mwaka huu Gwajima alitoa kauli ya kukemea utekaji. Kauli hiyo ilisababisha upinzani mkubwa kutoka ndani ya chama chake na kusababisha Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kusema:
“Tukitoa mwanya ndugu zangu, tukipitisha wanaotafuta tu na mie niwemo, ndiyo tunapata wale wanaokwenda huko. Chama kinakuwa Gwajimanised. Kwa hiyo kwa vyovyote vile tusi-Gwajimanise chama chetu, Magwajima tuyaache nje.”
Tangu wakati huo, Gwajima amepata misukosuko ikiwemo kanisa lake la Glory of Christ Tanzania, maarufu Kanisa la Ufufuo na Uzima kufungwa kisha kuzingirwa na askari polisi wenye silaha.
Kuna kesi inaendelea Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga kufungwa kwa kanisa hilo
Maoni
Chapisha Maoni